Ni suala la muda tu, leo mabingwa wa Tanzania Bara Yanga wanatarajia kukutana na Vital'O kutoka Burundi katika mechi ya kwanza ya hatua ya awali ligi ya mabingwa itakayochezwa kuanzia sa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam
Vital'0 ndio wenyeji wa mechi hiyo baada ya kukosa uwanja wenye sifa ya kutumika katika michuano hiyo inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) huko nyumbani kwao
Kuelekea mechi hiyo, Rais wa Yanga, Hersi Said, alisema msimu huu wanataka kuchukua kila kikombe cha mashindano ambayo watashiriki lakini akisisitiza ikiwamo ubingwa wa Afrika
Hersi alisema Yanga wanahitaji kutwaa taji hilo na wala si kufika hatua ya robo au nusu fainali ya michuano hiyo inayofanyika kila mwaka. Rais huyo alisema kikosi walichonacho msimu huu kina uwezo wa kubeba kombe hilo kubwa Afrika
"Kila mashindano ambayo tunashiriki safari hii dhamira yetu ni kubeba kombe, tunaweka mguu katika mechi za Ligi ya Mabingwa, dhamira kubwa na kwa baraka za Mwenyezi Mungu kwa nini tusiwe timu ya kwanza Tanzania kuleta ubingwa wa Afrika?" alisema Hersi
Nae Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, alisema mechi hiyo haitakuwa rahisi lakini amezungumza na wachezaji wake jinsi gani ya kufanya na hasa kutumia vizuri nafasi za kufunga mabao zitakazopatikana ili kuondoka na ushindi
Gamondi alisema matokeo ya ushindi yatawaweka katika nafasi salama zaidi kuelekea mchezo wa marudiano
"Tunataka kucheza vizuri na kushinda vizuri pia, ili tusiwe na presha sana katika mechi inayofuata, tunataka mchezo unaofuata uwe rahisi, nadhani hili ndilo kubwa zaidi," alisema Gamondi