Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema kikosi chake kimekamilisha maandalizi kuelekea mchezo wa marudiano ligi ya mabingwa hatua ya awali dhidi ya Vital'o ambao utapigwa kesho Jumamosi katika uwanja wa Azam Complex, saa 1 usiku
Akizungumza katika mkutano na wanahabari kuelekea mchezo huo, Gamondi amesema licha ya ushindi wa mabao 4-0 ambao waliupata katika mkondo wa kwanza, bado wana dakika nyingine 90 za kupambana ili kupata matokeo yatakayowapa nafasi ya kusonga mbele hatua inayofuata
"Tunajiamini na matokeo tuliyopata mechi iliyopita lakini bado tunaheshimu kuwa tuna dakika 90 nyingine za kupambana, kipaumbele chetu ni kufuzu hatua unayofuata," alisema Gamondi
Aidha kutokana na upana wa kikosi chake Gamondi amesema katika mchezo huo kunaweza kuwa na mabadiliko machache ya wachezaji lakini jambo muhimu atatumia timu ambayo itapambana na kuhakikisha wanapata matokeo ya kuwavusha hatua inayofuata
"Tunawaheshimu wapinzani wetu, tunajua mchezo huu utakuwa tofauti na mchezo wa kwanza, ndio kunaweza kuwa na mabadiliko kidogo ya kikosi lakini lengo letu ni kuwa na mchezo mzuri na kupata matokeo ambayo yatatupa nafasi ya kusonga mbele"