Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema klabu ina malengo makubwa katika michuano ya ligi ya mabingwa msimu huu hivyo haiko tayari kuwaachia wachezaji wake muhimu
Akijibu maswali ya wanahabari kuhusu ofa ambazo Yanga imepokea kwa ajili ya mshambuliaji Clement Mzize, Kamwe amesema sio Mzize tu, kuna ofa zaidi wamepokea kuwataka wachezaji wao wengine
Lakini amesema Yanga imeweka msimamo kuwa hakuna mchezaji ataondoka katika msimu huu ambao wanataka kutwaa ubingwa wa Afrika
"Clement Mzize alisaini mkataba wa miaka miwili ndani ya Yanga, kwa hivyo ukiacha klabu zote zinazomtaka Mzize basi aliichagua Yanga. Pia ukiachana na wachezaji wote duniani, mpaka Yanga inampa mkataba Mzize basi ilimchagua baada ya kuona anafaa kuitumikia Yanga"
"Nitafutieni timu kubwa Afrika kama Al Ahly, Mamelodi na nyingine duniani kama Real Madrid ambayo inawaachia wachezaji wake muhimu kwenye kikosi"
"Basi sisi ndio kama hao, sisi ni wakubwa Afrika na tunataka kufanya vizuri Afrika. Mkataba wake unaishi mwishoni mwa msimu huu, lakini nawahakikishia Clement Mzize bado yupo sana Yanga, kama ndoto zetu mnataka Mzize aondoke Yanga basi jambo hilo haliwezi kutokea," alisema Kamwe
Kamwe amesisitiza kuwa Yanga ndio klabu sahihi kwa Mzize kwani inaendelea kumkuza akitokea timu ya vijana
Amesema timu zote zinazomtaka Mzize haziko katika ubora ambao Yanga iko wakati huu hivyo kwa wale wanaosema Mzize atakua kisoka zaidi kama atajiunga na Wydad au Kaizer Chiefs hawako sahihi kwani timu hizo hazishiriki michuano yoyote mikubwa barani Afrika
"Kaizer Chiefs walimaliza nafasi ya 10 msimu uliopita, hawashiriki hata super 8 ya Afrika Kusini. Wydad walimaliza nafasi ya 6, ndio kwanza wameanza project ya kujiimarisha"
"Sasa unasemaje mchezaji aliyecheza fainali ya kombe la Shirikisho la CAF na robo fainali ya ligi ya mabingwa katika misimu miwili iliyopita, atakwenda kukua kama atajiunga na timu ambazo hata hazishiriki michuano yoyote ya CAF?," alihoji Kamwe