Mshambuliaji wa zamani wa Yanga Fiston Mayele amefichua kuwa amekuwa akiwasiliana mara kwa mara na Rais wa Yanga Injinia Hersi Said
Jana Mayele alikuwa sehemu ya kikosi cha DR Congo kilichochuana na Ethiopia katika mchezo wa kuwania kufuzu Afcon 2025 akifunga moja ya mabao katika ushindi wa mabao 2-0 ambao DR Congo waliupata
Akizungumza na wanahabari baada ya mchezo huo uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa, mshambuliaji huyo wa Pyramids Fc amesema Hersi amefanya kazi nzuri ya kukiboresha kikosi cha Yanga huku akiwatakia kila la kheri waajiri wake hao wa zamani
"Injinia Hersi ni mtu ambaye huwa naongea nae kwenye simu, hata baada ya fainali alinipongeza na mimi nilimpongeza kwasababu amesajili wachezaji wazuri"
"Yanga wanacheza kwa morali na nawatakia kila la heri. Nilimwambia kwamba aendelee kupambana, watafanya vizuri," alisema Mayele
Licha ya kujijengea heshima kubwa akiwa Yanga, Mayele 'aliwatibua' wananchi baada kuwatuhumu baadhi ya viongozi kuwa wanachangia yeye kutofanya vizuri Misri aliposajiliwa na Pyramids
Hata hivyo Mayele aliwaomba radhi viongozi wa Yanga kutokana na tuhuma na kauli zake ambazo wengi walizitafsiri kama kukosa shukrani kwani ni Yanga iliyotengeneza jina lake
Kwa sasa mshambuliaji huyo 'amejipata' katika ligi kuu ya Misri akishika nafasi ya pili katika mbio za ufungaji bora baada ya kupachika mabao 17