Baada ya kuipeleka Yanga hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika kwa msimu wa pili mfululizo, Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi ametuma ujumbe kwa timu nyingine zilizofuzu hatua hiyo kujiandaa kukutana na Yanga yenye kiu ya ubingwa wa michuano hiyo
Akizungumza baada ya kuisambaratisha CBE SA kwa mabao 6-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa New Amaan Complex, Gamondi alisema Yanga inakwenda makundi pasipo kuhofia timu yoyote watakayopangwa nayo
"Lengo letu la kwanza ilikuwa kufuzu hatua ya makundi, nafurahia tumefanikisha hilo tena kwa ushindi mnono katika mechi za hatua hii ya awali"
"Sisi tuko tayari kushindana na tutakabiliana na yeyote katika hatua hii pasipo woga"
"Kama msimu uliopita tulicheza dhidi ya Al Ahly na Mamelodi Sundowns katika mechi zenye ushindani mkali pamoja na kumfunga CR Belouizdad hapa nyumbani, tumejipanga zaidi msimu huu na hatuhofii yeyote tukiwa malengo ya kufanya vizuri zaidi," alisema Gamondi
Droo ya hatua ya makundi itafanyika Oktoba 7, Cairo Misri ambapo Yanga itakuwa chungu cha 2
Timu ambazo zinaweza kupangwa na Yanga katika makundi ni Al Ahly, Mamelodi Sundowns, Esperance na TP Mazembe
Nyingine ni Al Hilal, Orlando Pirates, Sagrada Esperanca, AS FAR Rabat
Pia zimo MC Alger, Djoliba, Stade D'Abdijan na Maniema Union