Ni siku 10 zimesalia kabla ya mchezo wa kwanza wa ligi kuu ya NBC msimu huu kati ya Simba dhidi ya Yanga utakaopigwa Jumamosi, Oktoba 19 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Kwa msimu huu itakuwa mechi ya pili kuwakutanisha watani wa jadi ambao August 08 walichuana katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii, Yanga ikiibuka na ushindi wa bao 1-0
Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi anajivunia rekodi nzuri dhidi ya Simba kwani katika mechi nne alizokutana nao, hajapoteza (ndani ya dakika 90)
Dabi hii itakuwa mechi nyingine muhimu kwa Yanga katika mkakati wake wa kutetea ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo
Kwani kama Yanga itashinda mchezo huo halafu kushinda mchezo wake wa kiporo maana yake itakuwa na tofauti ya alama tano dhidi ya watani zao Simba
Simba watahitaji muujiza kuweza kuzirudisha alama hizo kwani watapaswa kushinda mechi zao huku wakiiombea Yanga ipoteze
Katika misimu ya karibuni Yanga imedhihirisha inapokuwa mbele kwa tofauti ya alama tano au zaidi, vijana wa mjini wanasema 'imeisha hiyo' kwani walikwenda moja kwa moja kubeba ubingwa