Meneja wa Yanga Walter Harrison amesema maandalizi kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya Simba yanaendelea vyema ambapo dhamira yao ni kuhakikisha wanaendeleza ubabe dhidi ya watani zao Simba
Jumamosi, Oktoba 19 Yanga itachuana na Simba katika mchezo wa ligi kuu ambao Wananchi watakuwa wageni
Nje ya maandalizi yanaendelea uwanja wa Bandari, Harrison amesema mchezo wenyewe umeongeza hamasa kwa wachezaji, ari na morali yao ikiwa kubwa
Amesema Yanga inajivunia kikosi chake chenye wachezaji wenye uzoefu na mechi hiyo na hivyo kufanya kila wanapokutana na watani zao hao kuwa bora
"Tumekuwa tukipata ushindi kwa siku za hivi karubuni tukicheza dhidi ya Simba, kikubwa kwetu viongozi mechi hii hatuhitaji kuhamasisha sana kama michezo mingine ambayo wachezaji wanakuwa wamejisahau au wanazichukulia kawaida"
"Kwa kiasi kikubwa wachezaji wetu wengi wameshacheza mechi hizi, hawahitaji sana kuelezwa, hakuna asiyefahamu ukubwa wa dabi. Wenyewe wanajiandaa na kila mmoja anataka kupata nafasi ili aonyeshe alichonacho akijua ataangaliwa na watu wengi uwanjani na kupitia televisheni. Kwa hiyo haiitaji sana kuizungumza, yenyewe inajizungumza"
"Tuko katika maandalizi makali, tunaweka kila juhudi inayotakiwa kuhakikisha tunashinda. Huu ni mchezo mkubwa unaobeba hisia, lakini una pointi tatu tu, utofauti ni uhasimu tu uliopo, hii ni ligi yenye michezo 30, hata kama tukishindwa kupata matokeo mazuri, tunaweza kucheza mechi nyingine tukashinda, tukawa mabingwa," alisema Harrison
Yanga ilishinda mechi zote mbili za ligi dhidi ya Simba msimu uliopita ikifunga jumla ya mabao 7-1
Msimu huu tayari timu hizo zimekutana katika nusu fainali ya Ngao ya Jamii, Yanga ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 na baadae kuifunga Azam Fc mabao 4-1 katika mchezo wa fainali na kutwaa Ngao hiyo
Yanga imeshinda mechi tatu mfululizo dhidi ya Simba na inakwenda katika mchezo wa Jumamosi ikipewa nafasi kubwa ya kushinda