Kesho Jumamosi Yanga itashuka uwanja wa Azam Complex, Chamazi kuwakabili Azam Fc katika mchezo wa ligi kuu ya NBC
Kikosi cha Yanga kimetokea visiwani Zanzibar ambako juzi kilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Singida Black Stars na kupanda kileleni mwa msimamo wa ligi kwa mara ya kwanza msimu huu
Ni ratiba ngumu kwa Wananchi ambao kwa wastani wameshuka dimbani kila baada ya siku tatu huku wapinzani wao Azam Fc wakiwasubiri kwa takribani wiki nzima bila ya kucheza mechi ya ligi
Jambo la kujivunia kwa Yanga ni kuwa wachezaji wako tayari kucheza wakati wowote na pengine hii ndio sababu iliyowafanya washinde mechi zote nane msimu huu
Kesho Yanga itaingia dimba la Azam Complex ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza dhidi ya Azama Fc mara ya mwisho timu hizo zilipokutana kwenye ligi
Ilikuwa March 17 2023 Yanga ilikubali kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Azam Fc katika uwanja wa Benjamin Mkapa wananchi wakikumbuka mchezo huo uliopelekea majeraha kwa nyota wao Pacome Zouzoua na Yao Kouassi ambao baadae walikosa mechi ya robo fainali ligi ya mabingwa dhidi ya Mamelodi Sundowns
Licha ya Yanga kuifumua Azam Fc mabao 4-1 katika mchezo wa fainali ya Ngao ya Jamii, mchezo wa kesho una umuhimu mkubwa zaidi kwani kama Yanga itaibuka na ushindi, itajiweka katika nafasi nzuri kutetea ubingwa kwa msimu wa nne
Baada ya mchezo dhidi ya Azam Fc, Yanga itakuwa imemalizana na wapinzani wake wote katika mbio za ubingwa angalau kwa mzunguuko huu wa kwanza