Ligi Kuu ya NBC inaendelea leo ambapo vinara wa ligi hiyo Yanga ambao pia ni mabingwa watetezi, watakuwa dimba la Azam Complex kupepetana na Azam Fc
Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na rekodi ya aina yake msimu huu. Wananchi wameshinda mechi zote nane walizocheza huku ikiwa timu pekee ambayo haijapoteza mchezo wala kuruhusu bao
Hii itakuwa mara ya pili kwa Yanga na Azam Fc kuchuana na katika kipindi cha miezi miezi mitatu kwani timu hizo zilikutana katika mchezo wa fainali Ngao ya Jamii mwezi August na Yanga kutwaa Ngao hiyo kwa ushindi wa mabao 4-1
Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema mara nyingi mchezo dhidi ya Azam Fc hautabiriki lakini wanakwenda kucheza wakiwa imara na lengo lao ni kushinda
Gamondi alidokeza kikosi chake leo kitakuwa na mabadiliko ya wachezaji na hata kimbinu kwani atawakosa baadhi ya wachezaji ambao walipata majeraha katika mchezo uliopita dhidi ya Singida Black Stars
Yanga imekosa muda wa kutosha wa 'recovery' kwa wachezaji wanaopata majeraha kwani kwa wastani imekuwa ikishuka dimbani kila baada ya siku tatu tangu Oktoba 19 ilipoichapa Simba bao 1-0
Ni mchezo ambao pia Yanga inakwenda kucheza huku ikiwa na kumbukumbu Azam Fc ndio timu iliyowafunga kwa mara ya mwisho kwenye ligi kuu msimu uliopita
Baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Azam Fc March 17 2023, Yanga haijapoteza mechi nyingine yoyote ya ligi ikicheza mechi 17
Mtanange huo utapigwa saa 12 jioni