Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema anajivunia ubora wa kikosi chake na anaamini vijana wake watarejea na nguvu kubwa baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Azam Fc
Yanga imerejea mazoezini kujiandaa na mchezo dhidi ya Tabora United utakaopigwa Alhamisi Novemba 07 katika uwanja wa Azam Complex
Gamondi amesema kipigo hicho ni kama kimeongeza ari na chachu ya kupambana kwa wachezaji wake ambao wanapenda kuwa bora kila siku
"Najivunia kikosi changu kina wachezaji wenye uchu wa mafanikio, tumeumia pamoja kupoteza dhidi ya Azam lakini bado wananipa imani kuwa hawajakata tamaa na wanahitaji kuwa bora zaidi," alisema Gamondi
Aidha kocha huyo raia wa Argentina amesema hatabadili aina yake ya uchezaji licha ya changamoto anayokutana nayo msimu huu timu nyingi zikiweka idadi kubwa ya wachezaji nyuma kila zinapocheza dhidi ya Yanga
"Nimezungumza hili mara nyingi, siwezi kubadili muundo wa uchezaji wa timu yangu hata kama tukiwa pungufu uwanjani kwani naamini katika ushambuliaji"
"Nimekuwa nikikutana na changamoto ya timu nyingi pinzani kucheza kwa kujilinda muda mwingi, na kutunyima nafasi za kufunga, hili nalishughulikia,β aliongeza Gamondi