Yanga inahusishwa na mlinzi wa pembeni wa Singida Big Stars Israel Mwenda. Huu unaweza kuwa usajili wa dharura kutibu changamoto zinazoikabili Yanga katika safu ya ulinzi hasa upande wa kushoto
Mwenda ni mlinzi kiraka ambaye anaweza kutumika upande wa kulia na hata kushoto. Mchezaji huyo alijiunga na Singida BS mwanzoni mwa msimu huu akitokea klabu ya Simba aliyoitumikia kwa misimu minne
Inafahamika ni ngumu kwenye dirisha dogo kupata wachezaji wa daraja la juu sokoni kwa sababu wengi bado wana mikataba
Aidha ni timu chache ambazo zinaweza kuwa tayari kuachana na wachezaji muhimu katikati ya msimu
Singida BS wanaonekana kujitosheleza katika walinzi wao wa pembeni hivyo ni rahisi kwao kumruhusu Mwenda akaitumikie Yanga kwa mkataba wa muda mfupi
Yanga na Singida BS ni timu zenye mahusiano mazuri, wachezaji kama Metacha Mnata, Zawadi Mauya na Joseph Guede walikuwa sehemu ya kikosi cha Yanga msimu uliopita, sasa wako Singida BS
Yanga pia inatajwa kukamilisha usajili wa kiungo mkabaji Kelvin Nashon nae kutoka Singida BS. Huu pia ni usajili wa dharura kwa ajili ya 'kuziba mashimo'
Khalid Aucho amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara huku Aziz Andabwile akipata majeraha ambayo yanaweza kumuweka nje kwa muda mrefu
Bahati mbaya kwa Jonas Mkude hajamshawishi kocha mpya wa Yanga Sead Ramovic ambaye amelazimika kumbadilishia majukumu Duke Abuya kutoka kiungo cha ushambuliaji na kuwa kiungo mkabaji
Unaweza kusema anapokosekana Aucho Yanga inakosa kiungo mkabaji wa asili kwani hata Mudathir Yahya na Salum Abubakar sio aina ya viungo ambao wanaweza kubaki pale nyuma kulinda safu ya ulinzi
Pengine hii ndio sababu ya Yanga kwenda Singida BS kumuomba Nashon ambaye licha ya kuwa hapati nafasi mara kwa mara kwenye kikosi cha Singida BS, ni kiungo mkabaji ambaye huwezi kumtilia mashaka kwani mara kadhaa ameitwa hata timu ya Taifa