Kocha Mkuu wa Yanga Sead Ramovic ameeleza kufurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mashujaa Fc uliopigwa uwanja wa KMC Complex jana na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-2
Ramovic amesema taratibu timu yake imeanza kuimarika na kucheza aina ya soka analohitaji ingawa bado kuna mapungufu yanayohitaji maboresho
"Niwapongeze wachezaji wangu, tumekuwa na mchezo mzuri sana leo (jana), pengine tulistahili kupata ushindi mnono zaidi"
"Dakika 25 za kwanza tulikuwa bora zaidi na kutengeneza nafasi nyingi tungeweza kufunga hata mabao matano lakini tulitumia nafasi mbili tu"
"Baada ya hapo tulipunguza kasi, kama nilivyosema awali mahitaji ya kimbinu ya mchezo wetu yanahitaji 'fitness' kubwa, bado wachezaji wangu hawajafikia katika kiwango hicho na ndio maana tunafanya kazi kubwa katika uwanja wa mazoezi"
"Naamini tuko katika mwelekeo sahihi baada ya muda tutakuwa na timu iliyobora zaidi," alisema Ramovic
Yanga iliuanza mchezo huo kwa kasi, 'Gusa, achia twende kwao' ilionekana mapema Yanga ikifunga mabao mawili ya haraka kupitia Prince Dube kabla ya Ulomi kufunga bao la kwanza la Mashujaa akipiga shuti la chini nje ya 18 ambalo lilimshinda mlinda lango Aboubakar Khomein
Yanga ikarejea tena na kasi katika kipindi cha pili Dube akiongeza bao la tatu nae Stambuli kuifungia Mashujaa bao jingine kutoka nje ya 18