Kocha Mkuu wa Yanga Sead Ramovic amesema wamejiandaa kikamilifu kwa mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya TP Mazembe ambao utapigwa kesho Jumamosi katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Akizungumza katika Mkutano na wanahabari mapema leo, Ramovic alisema Yanga inakwenda katika mchezo huo ikiwa katika kiwango bora na watapambana ili kuhakikisha wanashinda na kuendelea kubaki katika malengo ya kufuzu robo fainali
Ramovic amebainisha kuwa amepata muda mzuri wa kukiandaa kikosi chake ambapo baada ya wiki nne za mazoezi anaamini wachezaji wake wako katika wakati bora zaidi kuliko wakati anakabidhiwa timu
"Tunayo mechi muhimu sana mbele yetu, na tunajua tunahitaji alama tatu ili bado tuwe na nafasi ya kufuzu kwa raundi inayofuata"
"Nilipofika wiki nne zilizopita, niliona kwamba timu haikuwa fiti kabisa, na hiyo ndiyo ukweli. Sasa katika hizi wiki nne lazima niwape sifa nyingi wachezaji wangu jinsi walivyofanya kazi, jinsi walivyovumilia kila siku kufikia kiwango ambacho ningependa kuwaona. Na tuna furaha kubwa kucheza mechi ya kesho tukiwa kwenye hali nzuri dhidi ya TP Mazembe"
"Pengine watacheza kwa mtindo ule ule waliocheza kwenye mchezo wa kwanza dhidi yetu. Kwa mipira ya juu, kushinda mipira ya pili, na kurusha krosi nyingi kwenye eneo letu. Tutakutana na mechi ngumu lakini tumejiandaa vizuri kwa sababu tuna wachezaji binafsi wenye uwezo mkubwa na tumeanza kuwa timu. Hili linanifanya nijivunie sana kama Kocha," alisema Ramovic
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, nahodha msaidizi wa Yanga Dickson Job alisema wachezaji wote wako tayari na watapambana ili kuhakikisha wanashinda
"Kwa niaba ya wachezaji wenzangu tupo kwenye wakati mzuri kitumu, tunajua umuhimu wa mchezo wa kesho na tutakwenda kupambana asilimia 100 kuhakikisha tunapata matokeo"