Licha ya kuwa tayari wamefuzu robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika, Al Hilal hawatakuwa wepesi pale watakapokutana na Yanga siku ya Jumapili Januari 12 katika mchezo wa raundi ya tano kundi A
Yanga iliondoka jijini Dar es salaam mapema leo wakielekea Mauritania kupitia Istanbul, tayari kwa mchezo huo ambao unaweza kuamua hatma ya Yanga katika kuwania tiketi ya kufuzu robo fainali
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema wachezaji na benchi la ufundi wanafahamu ugumu wa mchezo wa Jumapili
"Inaweza kuonekana mechi itakuwa nyepesi kwa sababu Al Hilal tayari wamefuzu lakini sio hivyo. Mpaka sasa Al Hilal wana uhakika wa kucheza robo fainali lakini hawana uhakika kama wataongoza kundi"
"Sote tunafahamu faida ya kuongoza kundi, kwenye robo fainali unacheza dhidi ya timu iliyomaliza nafasi ya pili kundi jingine na utaanzia ugenini na kumalizia nyumbani"
"Mchezo dhidi ya Yanga utakuwa wa mwisho kwa Al Hilal kucheza nyumbani. Mechi yao ya mwisho makundi watahitimisha dhidi ya TP Mazembe DR Congo"
"Hivyo utaona ni kwa kiasi gani watahitaji kushinda mchezo dhidi yetu au kupata sare ili kuwa na uhakika wa kuongoza kundi"
"Lakini nasi kwa upande wetu tunazihitaji alama tatu za mchezo huu na si vinginevyo. Hivyo tunakwenda Mauritania huku kila mmoja akifahamu kazi kubwa iliyo mbele yetu," alisema Kamwe
Kama Yanga itaibuka na ushindi dhidi ya Al Hilal, basi itahitaji ushindi mwingine wa aina yoyote nyumbani dhidi ya MC Alger ili kufuzu robo fainali
Mechi ya mwisho dhidi ya MC Alger itapigwa Januari 18 katika uwanja wa Benjamin Mkapa