Kwa sasa Yanga imewekeza nguvu katika kutetea mataji yake mawili ya ligi kuu na kombe la Shirikisho la CRDB ambapo Jumamosi kampeni ya kutetea taji la CRDB itaanza uwanja wa KMC Complex katika mchezo wa raundi ya pili dhidi ya Copco Fc ya Mwanza
Baada ya mchezo huo Wananchi wanahamishia nguvu katika ligi kuu ambapo Februari 1 Yanga itashuka dimba la KMC Complex kuikabili Kagera Sugar
Yanga itacheza mechi tano mfululizo jijini Dar es salaam ambapo kama kocha Sead Ramovic atachanga karata zake vyema, kuna alama 15 ambazo Yanga inaweza kuzikusanya kabla ya kusafiri mkoani Kigoma kuikabili Mashujaa Fc
Mechi tano zinazofuata jijini Dar es salaam ni dhidi ya Kagera Sugar, KenGold (zinapigwa KMC Complex), JKT (Meja Jen. Isamuhyo), KMC, Singida BS zote zikipigwa KMC Complex
Katika duru ya pili Yanga itakuwa na mechi tano nje ya mkoa wa Dar es salaam wakianza na Mashuja (Feb 23) na Pamba Jiji (Feb 28)
Machi 08 Yanga itakuwa mwenyeji wa Simba uwanja wa Benjamin Mkapa katika dabi ya pili kwenye ligi msimu huu, mechi ambayo inaweza kuamua hatma katika mbio za ubingwa
Baada ya mchezo dhidi ya Simba, kituo kitakachofuata ni Tabora United dimba la Ali Hassan Mwinyi (April 1) katika mechi ya kisasi kwa Yanga
Baadae Yanga itarejea Dar kucheza mechi nyingine mbili dhidi ya Coastal Union (April 7) na Azam Fc (April 10) hii ikiwa mechi nyingine ya kisasi kwa Yanga
Baada ya mechi hizo Wananchi watasafiri Manyara kuikabili Fountain Gate (April 20) kisha kurejea Dar kuikabili Namungo Fc (May 13)
May 21 Yanga itakuwa Mbeya kuhitimisha mechi ya mwisho ugenini msimu huu dhidi ya Tanzania Prisons kisha kurejea jijini Dar es salaam kwa ajili ya mechi ya kuhitimisha msimu dhidi ya Dodoma Jiji (May 25)