Rais wa Yanga Injinia Hersi Said amesema mpira ni biashara hivyo kuuziana wachezaji ni sehemu ya mahusiano ya klabu
Hersi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la vilabu Barani Afrika (ACA) jana alijibu maswali ya Wanahabari nchini Morocco baada ya kusaini makubaliano ya kukabidhiwa jengo la ofisi ya ACA
Wengi walitaka kujua kinachoendelea juu ya tetesi za usajili wa wachezaji Clement Mzize na Stephane Aziz Ki ambao wanawaniwa na klabu za Wydad na Raja CA
Hersi alisema ana mahusiano mazuri na marais wa klabu hizo na kama watakubaliana hakuna tatizo kufanya biashara
"Jambo muhimu kwetu kama klabu, tukikaa na kukubaliana tutafanya biashara, mpira ni biashara si ndio? Unapoona wachezaji wanahama kutoka timu moja kwenda nyingine ni sehemu ya uhusiano kati ya klabu"
"Mr Hicham (Rais wa Wydad) ni kaka yangu na namuheshimu sana hata Adil ambaye ni Rais wa Raja ni kaka yangu pia, tumetengeneza mahusiano ili kuhakikisha tunasaidiana," alisema Hersi
Mara kadhaa Wydad imetuma ofa Yanga kwa ajili ya kuwasajili Mzize na Aziz Ki huku Raja nao wakijitosa kumuwania Aziz Ki ambaye mwishoni mwa msimu uliopita aliongeza mkataba kuendelea kuitumikia Yanga kwa misimu mingine miwili