Ilikuwa mshituko sio kwa mashabiki tu, hata uongozi wa Yanga chini ya Rais Injinia Hersi Said ulishtushwa na uamuzi wa ghafla uliochukuliwa na kocha Sead Rmovic kusitisha mkataba wake ili kwenda kupata 'malisho' bora zaidi sehemu nyingine
Ndani ya uongozi na hata katika benchi la ufundi hakuna aliyekuwa akifahamu yaliyokuwa yakiendelea nyuma ya pazia baina ya Ramovic na CR Belouizdad kwani kocha huyo alifanya siri
Ramovic aliendelea na majukumu yake kana kwamba hakuna kinachoendelea. Ilipofika Jumanne saa 11 jioni ndipo Ramovic akatoa taarifa juu ya uamuzi wake wa kuondoka
Na alipokamilisha mazoezi ya mwisho akawaaga wachezaji huku akiwaacha wamepigwa na butwaa
Katika mkataba wake kulikuwa kipengele cha kununua mkataba huo, CR Belouizdad walikubali kulipa gharama hivyo hakuna kitu ambacho Injinia Hers angeweza kufanya kumzuia asiondoke
CR Belouizdad walimtangaza Ramovic jana kuwa Kocha wao Mkuu baada ya kukamilisha taratibu zote huku Yanga ikimuajiri Miloud Hamdi aliyekuwa akiinoa Singida Black Stars

Inaelezwa Ramovic alipewa ofa kubwa na CR Belouizdad ambapo mshahara wake ni karibu mara tatu ya ule aliokuwa akilipwa na Yanga
Katika upande huo hana lawama kwani katika kazi kila mmoja huangalia maslahi lakini angeweza kuwashirikisha viongozi wa Yanga ili wajipange kusaka mbadala wake kwani inaaminika mchakato huo haukuwa wa ghafla