Baada ya mchezo dhidi ya JKT Tanzania, hakuna muda wa kupoteza kwa Yanga kwani kikosi kinarejea mazoezini kujiandaa mchezo unaofuata dhidi ya KMC
Ijumaa ya wiki hii, Februari 14 Yanga itashuka KMC Complex katika mechi ya 'dabi' inayokutanisha timu zinazotumia KMC Complex
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amewataka mashabiki na wanachama wa timu hiyo kuendelea kuiunga mkono timu yao kwani dhamira ya kutetea ubingwa iko palepale
"Mechi hii (dhidi ya JKT Tanzania) imepita sasa tunajipanga kwa mchezo unaofuata Ijumaa dhidi ya KMC. Msimu huu kila mechi ina presha yake hivyo ukimaliza mechi moja haraka unapaswa kusahau kilichotokea na kujipanga na mchezo unaofuata"
"Leo (jana) hatukuwa na mchezo mzuri sana, nafikiri kulikuwa na uchovu kidogo ndio maana wachezaji wetu walicheza na tempo ya chini sana lakini yote kwa yote tumekubalia matokeo na tunasonga mbele," alisema Kamwe
Licha ya kulazimishwa suluhu ya bila kufungana dhidi ya JKT Tanzania, Yanga imeendele kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 46
Bado mbio za ubingwa ni ngumu, kuna mechi 12 za kuendelea kupambana kutetea taji la ligi kuu