Kocha Mkuu wa Yanga Miloud Hamdi amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya KMC na wamejiandaa kushinda mchezo huo
Akizungumza katika mkutano na wanahabari mapema leo, Hamdi alisema anatambua mashabiki wa Yanga wanahitaji alama tatu hapo kesho baada ya kukosa ushindi katika mchezo uliopita
Amesema ari na morali ya wachezaji wote iko juu na wako tayari kwa mchezo huo wa raundi ya 19
"Kama timu tuko tayari na tutafanya kila linalowezekana ili kushinda mchezo dhidi ya KMC"
"Nafahamu mashabiki wetu hawana furaha baada ya kukosa ushindi katika mchezo uliopita lakini niwaambie tu hata upande wetu benchi la ufundi na wachezaji walipambana kushinda mchezo dhidi ya JKT Tanzania lakini tulikosa bahati"
"Mchezo uliopita tulicheza dhidi ya timu ambayo ilikaa nyuma kwa zaidi ya asilimia 80 ya mchezo, tumejiandaa kukabiliana na aina hiyo ya mchezo, tutahitaji kuwa makini na utulivu ili kutengeneza nafasi na kufunga magoli," alisema Hamdi
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, nahodha wa Yanga Bakari Nondo Mwamnyeto amesema wachezaji wote wako tayari kuipambania Yanga kupata ushindi hapo kesho
"Mchezo uliopita tulipoteza pointi mbili, tumezungumza wachezaji wote na kukubaliana kesho lazima tupambane kupata ushindi"
"Kila timu inayocheza na Yanga wachezaji wake wanajitoa kwa asilimia 100 hivyo nasi tumejipanga kukabiliana na KMC lengo ni kupata pointi 3," alisema Mwamnyeto