Ni takribani wiki mbili na siku kadhaa zimebaki kuelekea mchezo wa duru ya pili Kariakoo Derby kati ya Yanga dhidi ya Simba
Mechi itapigwa uwanja wa Benjamin Mkapa March 08. Hii unaweza kusema ni mechi ya maamuzi kuelekea ubingwa wa ligi kuu msimu huu
Yanga imejipanga kutetea taji hilo kwa msimu wa nne lakini ili kufanikisha hilo ni lazima Wananchi washinde mchezo huo
Achana na mechi yenyewe, kuna sintofahamu juu ya waamuzi ambao watapewa kuchezesha mchezo huo
Msimu huu mechi mbili za Kariakoo Derby tayari zimepigwa, zikichezeshwa na Elly Sassie (Ngao ya Jamii) na Ramadhani Kayoko (duru la kwanza)
Hata hivyo mechi hizo ni kama ziliwaponza waamuzi hao kwani hawaonekani mara kwa mara wakichezesha tena mechi za ligi kuu
Mwamuzi bora Tanzania kwa sasa Ahmed Arajiga ndiye anayeonekana kukidhi vigezo vyote vya kuchezesha mchezo huo lakini anaonekana akipewa mechi zinazohusisha klabu ya Yanga na nyingine tu lakini sio Simba! Ni kama Simba wamemgomea mwamuzi huyo kuchezesha mechi zao na wamesikilizwa!
Bodi ya ligi itapaswa kuwa makini katika uchaguzi wa waamuzi wa kusimamia mchezo huo, na kama kuna ulazima sio dhambi kwenda nje ya nchi kuchukua waamuzi 'neutral' ambao hawatakuwa na upande
Misri wamekuwa na utaratibu huo wa kuchukua waamuzi kutoka nje ya nchi kuchezesha mechi kati ya Al Ahly dhidi ya Zamalek lengo likiwa kukwepa upendeleo na 'kubebana'
Kwa aina ya waamuzi tulionao, na kwa kuzingatia presha ya mchezo huo pengine kuna ulazima wa kufuata utaratibu wa Misri
Ikumbukwe hii ni mechi inayobeba hisia za Watanzania na inagawa nchi katika pande mbili. Sasa ikitokea mwamuzi akachezesha kwa lengo la kuibeba timu moja ni jambo la hatari na linaweza kusababisha maafa