Baada ya kupata nafasi ya kucheza kwa takribani dakika 20 katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Pamba Jiji, winga wa Yanga Jonathan Ikangalombo ameonyesha yuko tayari kwa nafasi nyingine katika mchezo ujao dhidi ya Simba utakaopigwa March 08 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Tangu asajiliwe na Yanga Ikangalombo amecheza mechi moja tu, kutokana na mapendekezo ya benchi la ufundi kuwa mchezaji huyo aliyetua kwa Wananchi akitokea klabu ya AS Vita alihitajika kuimarisha 'fitness' yake kabla ya kuanza kutumika
Dakika chache alizocheza katika mchezo dhidi ya Pamba Jiji zilitosha kuonyesha Wananchi wamepata 'winga wa maana' ambaye atakuwa msaada mkubwa kwa mabingwa hao wa nchi
Kocha Mkuu wa Yanga Miloud Hamdi alionyesha kufurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na Ikangalombo katika mchezo huo ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Hamdi alisema winga huyo alionyesha mwanzo mzuri, akithibitisha kwamba ni mchezaji anayestahili kuvaa jezi za timu hiyo, akionyesha ukomavu mkubwa wa kuhimili presha na ujasiri wa kufanya mambo makubwa ndani ya mechi ya kwanza.
"Nilikuwa nasema wakati wote ni mchezaji mzuri mwenye ubora mkubwa, muda ambao tulimpa ulikuwa mchache lakini nadhani watu waliokuwa na maswali wameona kuna kitu gani anacho," alisema Hamdi na kuongeza:
"Mechi ilivyokwisha nilimuita na kumwambia amefanya vizuri, lakini akaniambia anataka sana kucheza mechi ijayo dhidi ya Simba, nimemwambia asubiri tutaona nini tutaamua kwa kuwa hiyo ni mechi yenye hesabu nyingi, ila naamini hata akicheza atafanya kitu kikubwa kwa kuwa ni mchezaji mkubwa"