Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema hajapokea hukumu yoyote ya kufungiwa kutoka kwa Kamati ya Maadili hivyo kuwataka mashabiki na wanachama wa Yanga kupuuza tetesi zinazosambazwa mitandaoni
Kamwe amesema baada ya taarifa hizo kusambaa, klabu ya Yanga ilifanya jitihada kupata ukweli wake lakini mamlaka ilithibitisha haikutoa taarifa hizo
"Hakuna ukweli wowote juu ya taarifa hizo na sijui hao waliozisambaza walikuwa na lengo gani. Klabu ilifanya jitihada kupata ukweli wake na imebainika hakuna ukweli wowote"
"Naamini wenye mamlaka ya masuala ya mitandaoni (TCRA) wanaweza kuchukua hatua kwa wale waliosambaza taarifa hizi"
"Ni taarifa zilizoniletea changamoto kubwa kwani tangu juzi nililazimika kukesha hospitalini baada ya Mama yangu kupata mshituko," alisema Kamwe
Aidha Kamwe amesema imekuwa wiki ngumu kwake kwani kesi yake mbele ya Kamati ya maadili imevuruga mipango ya hamasa ya mchezo dhidi ya Simba
"Tulipanga kuanza hamasa kuelekea mchezo dhidi ya Simba Jumatatu lakini haikuwezekana kwani kesi ilisikilizwa kwa siku mbili yaani Jumatatu na Jumanne"
"Siku ya Jumatano usiku ndio zikasambaa taarifa kuwa nimefungiwa, hivyo utaona kwa kiasi gani jambo hili lilivurugu mipango yetu ya hamasa," aliongeza Kamwe