Baada ya kuteleza katika michuano ya ligi ya mabingwa msimu huu, mabosi wa Yanga tayari wameanza kupiga hesabu kali kuelekea msimu ujao
Kuna maboresho yanatarajiwa kufanyika mwezi Juni ambapo mpaka sasa ni kama tayari maingizo mapya yamepatikana unasubiriwa muda tu
Moja ya maingizo yanayotarajiwa ni mshambuliaji wa Singida Black Stars Jonathan Sowah ambaye alitua kunako timu hiyo katika dirisha dogo
Ndani ya muda mfupi, Sowah ameuwasha moto kwelikweli akipachika mabao 7 katika mechi 7 alizoitumikia Singida BS kwenye ligi
Katika moja ya mahojiano yake, alifichua kwake kuitumikia Yanga ni suala la muda tu kwani Rais wa Yanga Injinia Hersi Said ni kama baba yake na alimshukuru kwa kufanikisha ujio wake Tanzania
Kama Sowah anatua, maana yake Yanga italazimika kukata jina la mchezaji mmoja wa kigeni ili kuchukua nafasi yake
Hata hivyo kuna baadhi ya nyota wanamaliza mikataba na wengine bado mazungumzo ya kuhuisha mikataba yao hayajaanza
Mshambuliaji Kennedy Musonda na viungo Khalid Aucho na Clatous Chama ni miongoni mwao
Aucho bado ni mchezaji muhimu katika kikosi cha kocha Miloud Hamdi hivyo ni wazi ataongezwa mkataba
Wachezaji wengine kama Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua na Yao Kouassi mikataba yao inamalizika pia lakini imeelezwa tayari nyota hao wameshafikia mwafaka wa mikataba mipya
Chama alisaini mkataba wa mwaka mmoja katika dirisha lililopita Julai, lakini hajawa na nafasi katika kikosi cha kwanza pengine hatma yake kama ilivyo kwa Musonda itaamuliwa na mapendekezo ya benchi la ufundi lakini unaweza kusema pengine ndio wachezaji ambao nafasi zao zinaweza kuwa kwenye hatihati