Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi ameweka wazi ili kutetea ubingwa ligi kuu ya NBC msimu huu, hawana namna nyingine zaidi ya kushinda kila mechi hivyo kikosi chake kinahitaj kuifunga Tabora United hapo kesho
Hamdi ameweka wazi anafahamu Yanga ilipoteza mechi ya kwanza dhidi ya Tabora United iliyopigwa jijini Dar es salaam hivyo matumaini ya wanachama na mashabiki wote wa Yanga ni kuona wanashinda mchezo huo na kulipa kisasi
Amesema wachezaji wa Yanga wanalielewa hilo na amewapa kazi ya kufanya ili wanachama na mashabiki kuwa na furaha baada ya maumivu waliyoyapata kwenye mchezo wa kwanza
"Tunajua Tabora United ni timu ngumu, lakini lazima tukapambane. Tuna malengo makubwa ya kuwania ubingwa hivyo tunapaswa kushinda kila mechi inayokuja mbele"
"Nafahamu Tabora United walitufunga katika mechi ya kwanza, tumejipanga kuhakikisha hilo halijitokezi tena katika mechi inayofuata"
"Najua mashabiki wetu watakuja kwa wingi kutuunga mkono kama wanavyofanya katika mechi zote, sisi tutapambana kwa ajili yao kuwapa furaha," alisema
Kikosi cha Yanga kiliondoka jijini Dar es salaam Alfajiri ya leo Jumanne kuelekea Tabora tayari kwa mchezo huo utakaopigwa Jumatano, saa 10 jioni katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi