Alhamisi April 10 Yanga inarudi uwanja wa Azam Complex kumenyana na Azam Fc katika mchezo wa ligi kuu ya NBC
Unaweza kusema hii ni mechi muhimu kwa Wananchi kwani matokeo ya ushindi yatazidi kuisogeza Yanga karibu na ubingwa wa 31
Lakini pia itakuwa ni mechi ya kisasi kwa Yanga baada ya kupoteza mchezo wa duru ya kwanza wakifungwa bao 1-0 hapo Azam Complex
Baada ya vipigo dhidi ya Azam Fc na Tabora United, mabingwa hao watetezi ambao tangu msimu uliopita walitumia uwanja wa Azam Complex kama uwanja wao wa nyumbani, walihamia KMC Complex
Tangu Yanga ilipohamia KMC Complex, imeshinda mechi zote zilizopigwa katika uwanja huo. Alhamisi wanarudi Azam Complex kucheza tena lakini safari hii watakuwa wageni
Ni mechi inayotarajiwa kuwa na upinzani mkali, Azam Fc hawana cha kupoteza kwani nafasi yao kutwaa ubingwa wa ligi kuu ni finyu lakini pia timu hiyo tayari imetupwa nje katika michuano ya kombe la Shirikisho la CRDB
Ikiwa imesalia na mechi tano kuhitimisha msimu huu, ushindi siku ya Alhamisi utaifanya Yanga iwe katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa
Baada ya mchezo dhidi ya Azam Fc, Yanga itasalia na mechi nne dhidi ya Fountain Gate (Manyara), Namungo (Dar), Tanzania Prisons (Mbeya) na Dodoma Jiji (Dar)
Akizungumza baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union jana, Kocha Mkuu wa Yanga Miloud Hamdi alisema mechi inayofuata dhidi ya Azam Fc atahitaji nguvu ya kila mchezaji na sapoti ya mashabiki ili kuhakikisha wanachukua alama zote tatu