Mshambuliaji wa Yanga Kennedy Musonda huenda akatua klabu ya Al Ittihad inayoshiriki ligi kuu ya Libya, imefahamika
Taarifa kutoka mtu wa karibu wa mshambuliaji huyo, imedokeza kuwa tayari Musonda amefikia makubaliano binafsi na Al Ittihad na anachosubiri ni kumalizika kwa mkataba wake na Yanga ili ajiunge na miamba hao wa Libya
Mkataba wa Musonda unafikia tamati mwishoni mwa msimu na mpaka sasa hakuna mazungumzo ya mkataba mpya
Musonda ameitumikia Yanga kwa misimu miwili na nusu tangu alipojiunga na mabingwa hao wa nchi akitokea klabu ya Power Dynamos ya Zambia
Majeraha ya mara kwa mara msimu huu yamemfanya asionekane dimbani huku washambuliaji Clement Mzize na Prince Dube wakionekana kufanya vizuri zaidi yake
Musonda alikuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa taji la Muungano Zanzibar wiki iliyopita, hata hivyo alicheza mechi moja tu ya robo fainali dhidi ya KVZ ambayo hata hivyo alishindwa kumaliza dakika 90 baada ya kuumia