Katika ulimwengu wa soka, mafanikio huja kwa bidii, nidhamu, na kipaji cha hali ya juu. Haya yote yanaonekana kwa mshambuliaji chipukizi wa Yanga SC, Clement Mzize, ambaye kwa sasa yuko kwenye kiwango cha juu kabisa akiwa na umri wa miaka 21 tu
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu ya Yanga, kuna dalili kubwa kuwa Mzize huenda akatimiza ndoto ya kucheza soka Ulaya, baada ya klabu kupokea ofa kutoka timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).
Kwa msimu huu wa 2024/25, Mzize anaongoza kwenye mbio za ufungaji bora akiwa na mabao 13, akidhihirisha uwezo wake wa kutisha mbele ya lango. Akiwa tegemeo ndani ya klabu yake ya Yanga na sasa akiwa anapata nafasi kwenye kikosi cha Taifa, jina la Mzize limeanza kuvuka mipaka ya Tanzania na kuwavuta macho ya mawakala na vilabu vikubwa vya barani Ulaya.
Nahodha wa Taifa Stars na mshambuliaji wa kimataifa, Mbwana Ally Samatta, ambaye kwa sasa anakipiga katika ligi kuu ya Uturuki na klabu ya PAOK, anaamini kuwa huu ndio wakati sahihi kwa Mzize kufanya hatua hiyo kubwa. Samatta amemsifu Mzize kwa utulivu wake uwanjani, uwezo wa kufunga, na namna anavyojitoa kwa ajili ya timu.
"Naamini Mzize ana nafasi nzuri ya kufanikiwa barani Ulaya, hivyo kama atapata timu huu ni wakati sahihi kwake," alisema Samatta.
Samatta ni mchezaji aliyewahi kupitia safari kama ya Mzize – kutoka ligi ya nyumbani hadi Ulaya, na kwa sasa ni mchezaji mwenye mafanikio makubwa akiwa miongoni mwa Wachezaji wa Kitanzania waliowahi kung’ara zaidi nje ya nchi.
Mzize amekuwa na msimu bora kabisa akiwa na kiwango cha juu. Ikiwa atapata nafasi ya kujiunga na timu ya Ligue 1, si tu atapata uzoefu wa kipekee, bali pia itakuwa fursa ya kukuza kipaji chake, kutimiza ndoto ya kucheza Ulaya na pia kuitangaza Yanga Kimataifa zaidi