Miongoni mwa wachezaji waliotoa mchango mkubwa kwa mafanikio ya Yanga msimu huu ni mlinda mlango wa kimataifa kutoka Mali, Djigui Diarra.
Ingawa alianza msimu kwa kusuasua kutokana na majeraha yaliyomuweka nje ya baadhi ya mechi za mwanzo, kurejea kwake kuliashiria mwanzo wa kipindi kingine cha utulivu na uimara kwenye safu ya ulinzi ya Wananchi.
Takwimu Zinazozungumza
Tangu arejee kikosini, Diarra ameonyesha kiwango kile kile cha hali ya juu kilichomfanya kuwa chaguo la kwanza langoni kwa misimu yote aliyohudumu Jangwani. Mpaka sasa, amekusanya cleansheet 15 katika mechi 21, wastani wa 0.76 cleansheet kwa kila mechi – kiwango cha juu sana kwa mlinda mlango yeyote katika ligi ya Tanzania Bara msimu huu.
Ili kuelewa uzito wa takwimu hizi, tunalinganisha na mpinzani wake mkubwa, Moussa Camara wa Simba SC, ambaye ana cleansheet 16 pia, lakini katika mechi 26, na hivyo kuwa na wastani wa 0.68 cleansheet kwa mechi.
Kama tungetegemea mantiki ya kiufundi katika utoaji wa tuzo ya Kipa Bora wa Msimu, kwa kuzingatia uwiano wa mechi na cleansheet, basi Djigui Diarra angekuwa tayari ameshaibeba tuzo hiyo.
Msimu uliopita, Diarra alipoteza tuzo hiyo kwa kipa wa zamani wa Coastal Union, Vumile Matampi, licha ya kuwa na msimu mzuri. Hili linaongeza kiu na ari kwake msimu huu, kushinda tuzo hiyo
Kwa sasa, Yanga inaongoza ligi ikiwa na alama 73, huku ikiwa na mechi mbili zilizosalia dhidi ya Tanzania Prisons na Dodoma Jiji. Yanga imeweka msimamo wa kutocheza mchezo dhidi ya Simba, Juni 15
Ni wazi Diarra atapambana kuhakikisha anamaliza msimu vyema katika mechi hizo zilizosalia