Kocha Mkuu wa Yanga Miloud Hamdi amesema maandalizi ya kikosi chake kuelekea mechi tatu za kuhitmisha msimu yanakwenda vyema
Baada ya mapumziko ya siku 10, Yanga ilirejea mazoezi mapema Jumatatu kwa ajili ya maandalizi ya mechi za kuhitimisha msimu ambapo Wananchi wanakabiliwa na mechi mbili za ligi kuu dhidi ya Tanzania Prisons na Dodoma Jiji na mchezo wa fainali ya kombe la CRDB dhidi ya Singida Black Stars
Hamdi amesema wachezaji wana kazi kwenye mechi mbili za Ligi Kuu Bara na ya fainali ya Kombe la Shirikisho (CRDB) ili wapate matokeo mazuri, huku akisisitiza wako tayari kwa ajili ya kuendeleza rekodi ya ushindi kama walivyoanza.
Kocha huyo aliwataja Pacome Zouzoua na Khalid Aucho kuwa wamerudi katika ushindani baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda wakiuguza majeraha waliyoyapata na kuwafanya wakosekane kwenye baadhi ya mechi zilizopita.
"Tuna kazi kubwa ya kufanya katika mechi mbili za ligi ambazo zimebaki. Tunaamini zitakuwa ngumu kutokana na timu ambazo tunakutana nazo kuhitaji ushindi pia hasa wenyeji wetu kwenye mchezo wa kwanza ugenini haipo kwenye nafasi nzuri inahitaji pointi tatu ili kujiweka katika mazingira ya kucheza na sisi tunazihitaji ili tutetee taji"
"Kikubwa kila mmoja kutimiza majukumu yake kwa wakati, ninaamini kwamba tutafanya vizuri na kupata matokeo mazuri kwenye mechi zetu zijazo kikubwa kinachonipa matumaini ni kurejea kwa wachezaji wangu ambao hata hivyo tayari wamerudi kwenye ushindani," alisema
Hamdi alisema ukiondoa wachezaji walioitwa timu za taifa na beki Yao Kouassi aliye majeruhi, wengine wote wapo kwenye hali nzuri na tayari kupambania pointi sita.
"Morali ipo juu na wanaendelea vizuri na maandalizi Juni 18 tutakuwa ugenini kuikabili Tanzania Prisons hautakuwa mchezo rahisi, lakini nina imani kubwa na jeshi langu lote lipo timamu isipokuwa Yao na tunaombea walioitwa timu za taifa warejee salama"
"Kurejea kwa Pacome na Aucho kumeongeza nguvu ukizingatia kuna mchezaji mmoja muhimu pia ameondoka kikosini Stephane Aziz Ki,” aliongeza Hamdi