Leo Jumatatu Juni 09 2025 saa 4 asubuhi viongozi wa Yanga wameitwa kuhudhuria kikao kilichoitishwa na bodi ya ligi (TPLB) kwa ajili ya kujadili hatma ya mchezo namba 184 ligi kuu ya NBC kati ya Yanga dhidi ya Simba ambao umepangwa kupigwa Juni 15 2025
Bodi ya ligi imeomba kukutana na viongozi wote wa Yanga yaani kuanzia Rais, Makamu wa Rais na Wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji
Yanga ilishatangaza msimamo wake wa kutoshiriki mchezo huo hadi pale madai yao ya kutaka majibu ya kwa nini haukufanyika March 08 yajibiwe
Lakini pia Yanga ilieleza kutokuwa na imani na viongozi wa Bodi na kutaka Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo Almas Kasongo na Mwenyekiti Steven Mguto waachie ngazi
Mpaka sasa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa, hakuna majibu ya nini kilipelekea mechi ya March 08 kuahirishwa na hakuna kiongozi yeyote wa Bodi aliyejiuzulu
Msimamo wa Wanachama wa Yanga kupitia matamko yaliyotolewa na viongozi wa Matawi na wazee wa klabu hiyo hivi karibuni, ni viongozi wao kutojihusisha kabisa na mchezo huo
Wanachama wameonya kiongozi yeyote ambaye atajaribu kuipeleka timu uwanjani pasipo madai yao kufanyiwa kazi basi atakuwa amejiondoa mwenyewe katika nafasi yake
Mpaka sasa Rais wa Yanga Injinia Hersi Said yuko Marekani akihudhuria kozi katika shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Havard hivyo ni wazi hatashiriki kikao hicho
Makamu wa Rais wa Yanga Arafat Haji ndiye anaweza kuongoza maafisa hao wa Yanga endapo watakwenda kushiriki kikao hicho