Katika kile kinachoonekana kama hatua ya kihistoria na ya kishujaa, Klabu ya Yanga imeamua kusimama kidete kutetea haki na usawa katika Ligi Kuu Tanzania Bara. Msimamo wa Yanga si kwa manufaa yao pekee, bali ni kwa ajili ya ukombozi wa vilabu vyote vinavyoshiriki ligi hiyo ni sauti ya mabadiliko ambayo soka la Tanzania limeisubiri kwa muda mrefu.
Kwa sasa, klabu nyingi zimeanza kufanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu, usajili wa wachezaji, benchi la ufundi na mifumo ya kiutawala. Ni wazi kwamba maendeleo haya yanapaswa kwenda sambamba na ubora wa ligi, ikiwa ni pamoja na usimamizi wa haki, uadilifu na uwazi katika maamuzi yanayoathiri matokeo ya michezo.
Lakini hali halisi ya ligi kwa sasa ni ya kusikitisha. Zipo timu zinazojichagulia waamuzi, kupanga matokeo, na kuendesha ligi kana kwamba ni mali yao binafsi. Hali hii imefanya soka la Tanzania kupoteza mvuto, mashabiki kupoteza imani hata wachezaji kukosa motisha. Ni udhalilishaji wa juhudi za vilabu vinavyojaribu kusonga mbele kwa haki.
Katika sakata linaloendelea kati ya Yanga na Bodi ya Ligi pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), ukweli unaanza kufichuka. Kilichokuwa kimefichwa kwa muda mrefu sasa kipo wazi, mfumo umejaa ubovu, upendeleo, na ukosefu wa uadilifu wa hali ya juu. Hatua ya Yanga inaweza kuwa mwanzo wa mabadiliko ya kweli.
Yanga, klabu kongwe iliyoasisiwa hata kabla ya uhuru wa nchi hii, imechukua jukumu la kihistoria kusema IMETOSHA. Huu ni msimamo wa kusafisha taswira ya ligi na kurejesha heshima ya mpira wetu. Ni wakati wa kuondoa kila aina ya urasimu, upendeleo, na matumizi mabaya ya madaraka ndani ya Bodi ya Ligi na TFF.
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi pamoja na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wameonesha wazi kushindwa kwao kulinda maslahi ya mpira wa miguu nchini. Ukimya wao mbele ya malalamiko ya klabu ni ishara ya kushindwa kwa mfumo mzima wa usimamizi. TFF kupitia kwa Katibu Mkuu wake pia imeonyesha udhaifu mkubwa kwa kushindwa kuchukua hatua mapema.
Taarifa ya Yanga iliyotolewa jana baada ya kikao baina yake na Bodi, imetoa mwanga juu ya kile kilichokuwa kikiendelea kwa muda mrefu. Malalamiko juu ya waamuzi yaliwekwa kapuni kwa sababu pengine waamuzi walikuwa sehemu ya mpango wa kuhakikisha timu fulani inanufaika. Huu ni uhuni ambao hauwezi kuvumiliwa tena.
Leo hii, Yanga siyo tu inatetea haki ya timu yake, bali imebeba matumaini ya klabu zote iwe ni kubwa au ndogo kwamba zama za uonevu zinaweza kufikia kikomo. Ni jukumu ambalo limechukuliwa kwa ujasiri mkubwa, na litabaki kuwa mfano wa kuigwa.
Kwa hatua hii ya Yanga, kuna matumaini makubwa kuwa misimu ijayo ya Ligi Kuu Tanzania Bara itasimamiwa kwa haki, itakuwa na ushindani wa kweli, na bingwa wa ligi atapatikana kwa juhudi za uwanjani, si kwa mipango ya mezani.