GEITA, Umoja wa Matawi ya wanachama wa Klabu ya Yanga mkoani Geita umeungana na Baraza la Wazee wa klabu hiyo katika kusisitiza msimamo wa kutocheza mechi ya dabi dhidi ya Simba SC, iliyopangwa kufanyika Juni 15, 2025, iwapo sababu za kuahirishwa kwa mchezo wa Machi 8 hazitatolewa pamoja na kutotimizwa kwa masharti yaliyotolewa na Yanga
Katika kikao kilichofanyika katika Tawi la Yanga kata ya Nyawilimilwa, wanachama hao walisisitiza kuwa wako nyuma ya maamuzi ya uongozi wa juu wa klabu, wakitaka taarifa kamili na wazi juu ya sababu za kuahirishwa kwa mchezo huo maarufu kama Dabi ya Kariakoo.
Mratibu wa Matawi ya Yanga mkoa wa Geita, Rajab Mohamed, alisema:
“Wanachama wa Yanga Geita hawataki timu iende uwanjani kama majibu ya kuahirisha mechi ya Machi 08 hayajatolewa. Hii Yanga si timu ya viongozi, ni timu ya wanachama.”
Rajab aliitaka Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kuacha kutumia kile alichokiita ubabe na badala yake kufanya tathmini ya kina na kushirikisha wadau katika kufanya maamuzi yanayoathiri mustakabali wa mpira wa miguu nchini.
Katibu wa Matawi ya Yanga Geita, Edmund William, aliongeza kuwa wanachama wao wanapongeza uongozi wa klabu na wazee kwa ujasiri wa kutoshiriki mechi hiyo hadi haki itakapopatikana.
“Tunaunga mkono uamuzi wa kutocheza ili Bodi ya Ligi ijifunze kuendesha ligi kwa haki na usawa bila kuumiza upande mmoja,” alisema Edmund.
Kwa upande wake, msemaji wa Tawi la Yanga Nyawilimilwa, Nkanga Malima, alisema:
“Hatuhitaji malumbano na mamlaka, tunahitaji majibu ya msingi. Hatma ya mchezo huu inategemea ukweli na uwazi wa taarifa ya Bodi.”
Klabu ya Yanga imeweka msimamo wa wazi kwamba haitashiriki mchezo wa dabi wala mechi nyingine zozote zitakazofuata, hadi pale TPLB na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) watakapowajibika na kutolea maelezo ya kina kuhusu sababu za kusitishwa kwa mechi ya awali