Kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu ya NBC, klabu ya Yanga SC itashuka dimbani bila kiungo wake mahiri Stephane Aziz Ki, ambaye alijiunga na miamba ya soka ya Morocco, Wydad Athletic.
Mchezo wa leo dhidi ya Tanzania Prisons utapigwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, na macho yote yatakuwa kwa mtu mmoja, Clatous Chama.
Wakati Yanga wakitafuta pointi muhimu ugenini, huko Marekani, Aziz Ki naye atakuwa akiitumikia Wydad Athletic dhidi ya Manchester City katika michuano ya Kombe la Dunia la Klabu.
Ni mwanzo mpya kwa nyota huyo wa Ivory Coast, lakini pia ni ukurasa mpya kwa Yanga, ambao sasa wanahitaji kujenga maisha bila mchezaji aliyekuwa roho ya kikosi chao katikati ya uwanja.
Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi, atalazimika kubadilisha mfumo wa kikosi chake kwa mara ya kwanza, huku nafasi ya Aziz Ki ikisubiri kujazwa.
Katika kikosi cha Yanga, jina linalojitokeza zaidi kurithi majukumu hayo ni la Clatous Chama, kiungo mshambuliaji mwenye uzoefu mkubwa na uchezaji wa kiwango cha juu.
Katika mazoezi ya mwisho kabla ya mchezo, Chama alionekana akifanya majukumu yote ambayo mara kwa mara yalikuwa yakifanywa na Aziz Ki, dalili kuwa Kocha Hamdi ana imani naye.
Huu unaweza kuwa wakati wa Chama kuthibitisha ubora wake kikamilifu akiwa tegemeo katika eneo la kiungo. Amezoea kuingia kama mbadala wa Aziz Ki, lakini sasa ana nafasi ya kuanza, kuongoza mashambulizi, na kuwa muunganisho wa kati ya kiungo na safu ya ushambuliaji.
Leo ikiwa siku ya kumbukumbu yake ya kuzaliwa, bila shaka siku hii itasindikizwa na furaha ya ushindi Mbeya
