Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Yanga Ali Kamwe amesema kipaumbele cha klabu kwa sasa ni kuhakikisha wanatetea taji la ligi kuu ya NBC kwa msimu wa nne mfululizo
Kamwe amesema kama klabu hawajawahi kuwa na malengo ya kutafuta tuzo binafsi kwa mchezaji mmoja mmoja bali ni malengo ya klabu yanayokuwa mbele na tuzo binafsi hufuatia zenyewe
Wakati huu Yanga ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi, inahitaji kushinda mechi mbili zilizobaki ili kutetea ubingwa huku washambuliaji wake Prince Dube na Clement Mzize wakiwa nyuma kwa tofauti ya mabao matatu katika mbio za ufungaji bora
"Kama klabu hatuna kipaumbele cha mtu binafsi, kipaumbele hapa ni timu na tunachopambania ni ubingwa halafu hizi tuzo binafsi zinakuja zenyewe. Sio kwamba timu inakwenda uwanjani ikamtengenezee magoli Dube, Pacome au Mzize"
"Timu inaingia uwanjani kwenda kutafuta pointi tatu, halijalishi tutazipata kwa ushindi wa goli moja bila ya kujali nani kafunga wanayanga watashangilia kwa sababu thamani ya hilo goli ni alama tatu ambazo ni kitu cha msingi"
"Msimu huu ukiisha, ikifika mwaka 2030 hatutakumbushana nani alikuwa mfungaji bora, bali tutakumbushana nani alikuwa bingwa. Kwa hiyo sisi nguvu yetu tumeiweka kwenye tuzo ya timu haya mengine yakija sisi tutafurahia halafu mwisho wa msimu tutapiga hesabu ya hizo tuzo binafsi." alisema Kamwe