Kocha Mkuu wa Yanga Miloud Hamdi leo anakwenda kwenye dabi ya Kariakoo akiwa na takwimu za aina yake tangu alipotua kwa Wananchi kuchukua mikoba iliyoachwa na Sead Ramovic
Katika mechi 12 za ligi ambazo Hamdi amekiongoza kikosi cha Yanga, ameshinda mechi 11 na kutoka sare mchezo mmoja huku kikosi chake kikifunga mabao 39 na kuruhusu mabao matatu tu
Lakini mechi ya leo dhidi ya Simba unaweza kusema inaweza kuwa mechi muhimu zaidi kwake kwani matokeo ya mchezo huo yanaweza kumpandisha thamani mara dufu mbele ya mashabiki wa Yanga au kumshusha
Kikosi chake leo kinahitaji ushindi dhidi ya Simba lakini hata akipata sare, itatosha kumuhakikishia kubeba taji la ligi kuu katika msimu wake wa kwanza ambalo litakuwa taji la nne mfululizo kwa Yanga
Ni wazi Hamdi atakwenda katika mchezo huo huku akichukua tahadhari kubwa na haitashangaza kama ataamua kuwaachia Simba wacheze mpira huku yeye akitumia mashambulizi ya kushitukiza
Bila shaka mlinda Djigui Diarra atarejea langoni baada ya kupumzishwa mchezo uliopita na hakutarajiwi kuwa na mabadiliko makubwa katika safu ya ulinzi
Chadrack Boka na Israel Mwenda wanaweza kuanza kama walinzi wa pembeni ingawa Kibwana Shomari anaweza kupewa nafasi mbele ya Isra ili afanye kazi maalum ya kumtuliza winga wa Simba Elie Mpanzu
Kibwana ni chaguo sahihi kama timu inaweka mkazo katika kulinda zaidi huku Isra akiwa bora zaidi katika kupeleka mashambulizi mbele
Msimu huu Mwenda amefunga mabao 3 na kutoa pasi 2 za mabao katika mechi 18 alizocheza ndani ya ligi kuu
Dickson Job na Ibrahim Bacca wanatarajia kulinda nafasi zao za mabeki wa kati huku Khalid Aucho na Mudathir Yahya ambao walikosa mchezo uliopita wakitarajiwa kurejea eneo la viungo wa ulinzi
Pacome Zouzoua, Clatous Chama na Maxi Nzengeli wanatarajiwa kuongoza safu ya viungo wa ushambuliaji huku Clement Mzize akitarajiwa kuanza kama mshambuliaji pekee
Licha ya kuimarika majeraha aliyopata katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons, Prince Dube hatarajiwi kuanza katika mchezo ambao unatarajiwa kuwa na kasi kubwa
Katika mkutano wake na wanahabari jana, Hamdi hakutaka kuweka wazi timu yake itaenda na mfumo gani katika mchezo huo, lakini akatoa tahadhari mfumo wake utategemea jinsi mpinzani wake atacheza
Hamdi alisema Yanga ina faida zaidi kuelekea mchezo huo kwa kuwa matokeo ya aina mbili yatatosha kuwapa ubingwa lakini ni tofauti kwa upande wa Simba ambao lazima washinde
Bila shaka zitakuwa dakika 90 za aina yake na burudani kwa mashabiki, hii ni kama mechi ya fainali hasa ikizingatiwa kombe litakuwa uwanjani