Kocha Mkuu wa Yanga Miloud Hamdi amesema wamejiandaa kuwapa furaha mashabiki wao visiwani Zanzibar kwa kushinda taji la CRDB mbele ya Singida Black Stars katika mchezo wa fainali utakaopigwa uwanja wa New Amaan Complex, kesho Jumapili
Akizungumza katika Mkutano na wanahabari mapema leo, Hamdi alisema anatarajia mchezo dhidi ya Singida BS utakuwa mgumu kwani nao hawakubahatisha kufuzu fainali kwani wana kikosi bora
Hata hivyo amesema jambo muhimu kwa Yanga ni kushinda taji hilo na kuwapa furaha mashabiki wao ambao wameiunga mkono timu hiyo tangu mwanzo wa msimu
"Kwanza niwapongeze Singida Black Stars kufika Fainali, hii siyo kwa bahati mbaya kwasababu wana kikosi kizuri sana. Kwetu sisi tunategemea mchezo mzuri na wenye Ushindani hapo kesho, tunatarajia kuwa na miongoni mwa mechi bora na ngumu"
"Kushinda taji kwaajili ya Wananchi ni jambo jema sana, tunajivunia hilo kwasababu wamekuwa wakitusapoti katika kila hali hivyo tupo hapa kupigana kwaajili yao, tupo hapa kuwapa furaha, Tunayarajia kesho watakuja kwa Wingi kwakuwa tunawahitaji sana"
"Wachezaji wangu wote wanajua umuhimu wa mchezo wa kesho,wana uzoefu wa kucheza mchezo kama huu, ninatarajia kesho watakuwa Wanajeshi bora watakaopambania Furaha ya Wananchi," alisema Hamdi
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, kiungo mshambuliaji Shekhan Khamis amesema wachezaji wote wako tayari kuipigania nembo ya Yanga katika mchezo huo na kuwapa furaha mashabiki wao
"Kwa niaba ya wachezaji wenzangu tupo vizuri na salama, tupo tayari kwaajili ya kuipambania timu yetu, tunawashukuru sana Mashabiki wetu kwakutupa hamasa kila wanapotuona, tunawaomba waje kwa Wingi hapo kesho ili tufurahi pamoja"
“Singida ni timu nzuri sana kila mtu anafahamu hili hivyo tunaamini utakuwa mchezo mgumu sana, niwaambie tu Wananchi kuwa sisi tupo tayari kwaajili ya kuipambania timu yetu, niwaombe waje kwa Wingi,” alisema Shekhan