Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Yanga Ali Kamwe amesema kuelekea maandalizi ya msimu ujao 2025/26 Yanga huenda ikacheza na timu inayoshiriki ligi kuu ya Uingereza
Akizungumzia maandalizi kuelekea pre-season hiyo, Kamwe amesema Yanga imealikwa katika nchi mbili kushiriki michuano maalum ya pre-season kama ilivyotokea msimu uliopita walivyoalikwa Afrika Kusini ambako walipata nafasi ya kucheza dhidi ya Ausburg inayoshiriki ligi kuu ya Ujerumani 'Bundesliga'
Kamwe amefichua katika moja ya mialiko hiyo wanaweza kucheza dhidi ya timu ya ligi kuu ya Uingereza
"Imetokea tu bahati mbaya wenzetu Kaizer Chiefs msimu huu hawajatualika kwenye Toyota Cup, lakini kulingana na taarifa niliyopata kutoka kwa Mtendaji Mkuu, klabu imepokea mialiko ya kushiriki pre-season katika nchi mbili tofauti lakini klabu pia ina mpango wa kwenda kufanya pre-season katika nchi mbili tofauti"
"Mialiko hii ina pre-season tournament ambazo klabu inashiriki na katika moja ya mialiko kuna timu ya ligi kuu ya Uingereza inashiriki hiyo tournament hivyo kama tutapata bahati ya kwenda kushiriki, tutacheza mechi nyingine kubwa"
"Mwaka jana tulicheza dhidi ya Ausburg na mwaka huu tunaweza kucheza na timu nyingine kubwa inayoshiriki ligi kuu ya Uingereza," alisema Kamwe
Akizungumzia mipango ya pre-season hiyo, Kamwe amesema wachezaji wataanza kurejea nchini mwishoni mwa mwezi Julai tayari kuanza pre-season itakayoanza mwanzoni mwa August
Msimu huu ligi kuu inatarajiwa kuchelewa kuanza kutokana na michuano ya CHAN itakayofanyika nchini mwezi August