Klabu ya Yanga SC ipo mbioni kumwongeza mkataba kiungo wake mahiri, Duke Abuya, raia wa Kenya, kufuatia kiwango bora alichoonyesha msimu uliopita.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema tayari mazungumzo yameshaanza ili kumwezesha kiungo huyo kusalia Jangwani kwa muda mrefu zaidi, huku mkataba wake mpya ukitarajiwa kuwa na maboresho.
Abuya, ambaye kwa sasa yuko mkoani Kilimanjaro kushiriki Tamasha la Kili Icons pamoja na mastaa wengine wa soka, amekuwa gumzo kubwa miongoni mwa mashabiki wa Yanga kutokana na mchango wake mkubwa uwanjani. Uhodari wake katika nafasi mbalimbali za kiungo ulimpa nafasi ya kipekee katika kikosi cha kocha Miloud Hamdi ambaye ametimkia Ismailia.
Mkenya huyo alijiunga na Yanga msimu uliopita kama mchezaji huru akitokea Singida Black Stars. Wakati usajili wake ukionekana wa kawaida mwanzo, wengi hawakutarajia kiwango kikubwa alichoonyesha katika msimu uliomalizika.
Uwezo wa Abuya kucheza nafasi nyingi kiwanjani, nidhamu, kasi na uelewa mkubwa wa mchezo ni mambo yaliyomfanya kuwa mchezaji muhimu katika safu ya kiungo ya Yanga. Kwa sasa, thamani yake imepanda maradufu.