Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kuanza maandalizi yake ya pre-season nchini Rwanda, imefahamika
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema wiki ya mwisho ya mwezi huu wachezaji wote wanapaswa kuwa wamerejea jijini Dar es salaam ambapo kabla ya kuondoka nchini, kutakuwa na zoezi la upimaji afya
Yanga imealikwa Rwanda kwenye Tamasha la Rayon Day ikitarajiwa kucheza dhidi ya Rayon Sports mchezo ambao utapigwa mwezi August katika tarehe ambayo itatangazwa baadae
Aidha kuna uwezekano Yanga ikaenda kuhitimisha pre-season yake Namibia ambako pia imepokea mwaliko wa kushiriki michuano maalum ya pre-season
Wenyeji wa michuano hiyo ni African Stars ambapo pamoja na Yanga, klabu nyingine zilizoalikwa ni Petro De Luanda na Lioli
Katika pre-season Yanga ina uhakika wa kucheza angalau mechi nne zenye hadhi ya Kimataifa kabla ya kurejea nchini kuhitimisha maandalizi yake kuelekea wiki ya Mwananchi
Hata hivyo Kamwe amesema huenda kukawa na ugumu kupata timu kubwa kuja kushiriki wiki ya Mwananchi kwani Septemba ligi nyingi zitakuwa zimeanza
Michuano ya CHAN inayofanyika nchini kuanzia August 2 hadi August 30 imepelekea Tamasha hilo kusogezwa mbele hadi Septemba
Kamwe amesisitiza kuwa Yanga imeiandikia barua Simba kuiomba kucheza nayo katika kilele cha Wiki ya Mwananchi na huku pia Yanga ikiwa tayari kwenda kucheza dhidi ya Simba katika Tamasha lao la Simba Day