Baada ya kutwaa mataji matano msimu uliopita, wengi wangedhani Yanga SC haina sababu ya kufanya usajili mkubwa katika dirisha hili.
Lakini tofauti na matarajio hayo, uongozi wa klabu chini ya Rais Injinia Hersi Said umeingia sokoni kwa nguvu zaidi, kusaka wachezaji wa daraja la juu yani ‘mashine za maana’ kuimarisha kikosi kilichoshinda kila kitu katika mashindano ya ndani msimu uliopita.
Lakini kwanini kuendelea kusajili wakati timu imetawala?
SIRI YA KUENDELEA KUWA BINGWA
Upo msemo maarufu kwamba “kutwaa ubingwa ni rahisi, lakini kuendelea kuwa bingwa ni kazi ngumu.” Ushindani wa ndani na nje huongezeka kila msimu, lakini pia changamoto ya wachezaji kushuka kiwango hasa wale wanaotumika kwa muda mrefu. Hii ndiyo sababu Yanga haijifungi kwenye mafanikio ya jana; badala yake, hutazama mbele kwa kujiuliza: nani atatufikisha mbali zaidi msimu unaofuata?
Injinia Hersi ameweka utaratibu wa wazi: kila msimu lazima kuwe na sura mpya ndani ya kikosi, huku tathmini ya mchango wa wachezaji ikifanyika kwa umakini mkubwa. Wachezaji wanaoonyesha mchango mdogo au waliokwisha kufikia kilele cha uwezo wao huondolewa kwa heshima, huku nafasi zao zikichukuliwa na wachezaji wenye njaa ya mafanikio.
Ukiangalia kikosi cha Yanga kilichotwaa ubingwa wa 2021/22, na kukilinganisha na kile kilichoshinda 2024/25 mabadiliko ni makubwa. Hata baadhi ya wachezaji waliokuwa bado na uwezo mzuri walipewa nafasi ya kuondoka ili kuleta nguvu mpya.
NYOTA WANAOONDOKA NA WANAOINGIA
Katika dirisha hili, nyota wakubwa kama Stephane Aziz Ki, Kennedy Musonda na hata Clatous Chama wameondoka. Lakini hii haimaanishi mwisho wa Yanga bali ni mwanzo wa sura mpya. Yanga iko sokoni kusaka mbadala wao, wachezaji wanaokuja si tu kujaza nafasi bali kuchochea moto uliodhoofika kidogo.
Wachezaji wapya wanapewa nafasi ya kuchangia maono ya Yanga: timu si ya mchezaji mmoja, bali mfumo unaojiboresha kila msimu.
MBINU YA KUJENGA TIMU YA KISHINDANI
Yanga imekuwa mfano wa klabu inayosimamia mpango wa ‘continuous improvement’. Mfumo huu wa kuingiza damu changa, kuboresha maeneo dhaifu na kuondoa wachezaji waliopungua ufanisi, ndiyo unaoweka Yanga mbele ya wapinzani wao.
Mafanikio ya Yanga hayajaletwa tu na wachezaji waliopo, bali na sera ya uongozi yenye kuona mbele: kuendelea kuijenga timu hata wakati ambapo kila mtu anaamini tayari iko kamili.