Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amekiri klabu hiyo kuwa katika mchakato wa kumsajili kiungo mahiri kutoka klabu ya CS Sfaxien ya Tunisia, Moussa Balla Conte
Kwa siku za karibuni Conte (21) ni mchezaji aliyezungumzwa zaidi katika tetesi za usajili ikidaiwa Yanga kumalizana na klabu yake ya CS Sfaxien huku watani zao Simba wakidaiwa kumalizana na mchezaji na hivyo kuibua sintofahamu kuhusu usajili wake
Kamwe amesema Conte ni kiungo mzuri amezivutia sio timu za Tanzania tu, bali hata klabu kama Pyramids na Esperance zinapambana kumsajili
"Mimi niseme wazi ni kweli Yanga tunamtaka Moussa Balla Conte, huyu ni kiungo mzuri ambaye amezivutia sio timu za Tanzania tu, pia Pyramids wanamtaka na hata Esperance"
"Ni kiungo mzuri ambaye anaweza kufanya mambo mengi uwanjani na zaidi umri wake bado ni mdogo, hivyo ni kweli Yanga tunamtaka"
"Sasa taarifa rasmi kama tumemsajili au la itafahamika kuanzia Julai 20 kwani ndio siku ambayo nitakabidhiwa faili la taarifa zote za usajili"
"Kuanzia tarehe 20 tutaanza kutoa taarifa zote, kocha mpya ni nani benchi la ufundi liko vipi, wachezaji waliomaliza mikataba yao na tuliyoivunja kwa makubaliano ya pande zote mbili na wachezaji ambao tumewasajili," alisema Kamwe
Aidha Kamwe amesema Yanga iko katika hatua za mwisho kukamilisha michakato yake ya usajili ambapo mpaka sasa ni mchezaji mmoja tu ambaye wanakamilisha usajili wake ili kufunga zoezi hilo
"Mpaka sasa usajili wetu umekamilika kwa asilimia kubwa, bado mchezaji mmoja tu kati ya wale tuliotaka kuwasajili ambaye tuko mwishoni kukamilisha usajili wake," aliongeza Kamwe