Mlinda lango Djigui Diarra kutoka Mali ameiheshimisha Yanga katika misimu minne ambayo amewatumikia Wananchi. Bahati mbaya haikuwa hivyo kwa beki Mamadou Doumbia ambaye alishindwa kutamba.
Taarifa ya duru za usajili imebainisha Wananchi wamerudi tena Mali, safari hii wamefuata kiungo mshambuliaji
Klabu ya Yanga inatajwa kujitosa kumuwania kiungo fundi Lassine Kouma (21), anayekipiga katika klabu ya Stade Malien
Kouma anayemudu vyema majukumu ya kucheza kama kiungo mshambuliaji namba 10, anaweza kutua Yanga baada ya mabingwa hao wa nchi kupiga hatua kubwa katika mazungumzo na Stade Malien, timu ambayo alitoka Diarra
Lakini sio Yanga tu, klabu ya Al Hilal ya Sudan na Simba ya Tanzania nazo ziko katika kinyang'anyiro cha kumuwania kiungo huyo
Kouma tayari ameutaarifa uongozi wa Stade Malien kuwa anahitaji changamoto mpya
Katika moja ya mahojiano yake, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe alisema bado kuna usajili wa mchezaji mmoja ambao wanapambana kukamilisha
Eneo la kiungo mshambuliaji limeendelea kuifanya Yanga iwe bize sokoni kusaka mchezaji ambaye atachukua mikoba iliyoachwa na Stephane Aziz Ki
Feisal Salum kutoka Azam Fc ni miongoni mwa wachezaji waliohusishwa kutua Yanga lakini inaonekana Azam Fc hawako tayari kumuachia, wanapambana kumuongeza mkataba akiwa miongoni mwa wachezaji ambao kocha mpya wa timu hiyo Florent Ibenge amewahitaji
Kuna majina kadhaa ambayo yamehusishwa na Yanga katika eneo hilo, kama watafanikisha usajili wa Kouma ni wazi itakuwa imefunga usajili wa nyota wa kigeni