Kocha Mkuu wa Yanga, Romain Folz, ameonyesha kuridhishwa kwake na kambi ya timu hiyo inayoendelea katika kituo cha Avic Town, eneo ambalo limekuwa ngome ya maandalizi ya Wananchi kwa misimu minne mfululizo.
Yanga iliingia Avic Town juzi, baada ya kutumia wiki mbili za mwanzo kujifua katika Uwanja wa KMC Complex. Katika kipindi hicho, Avic Town ilikuwa ikipitia ukarabati mkubwa, uliokuwa sababu ya kikosi kuchelewesha kurejea kambini hapo. Sasa ukarabati huo umekamilika, na Folz pamoja na benchi lake la ufundi wameridhia kuendelea na maandalizi hapo.
Awali, kulikuwa na tetesi kwamba Yanga wangeelekea nje ya nchi mara baada ya mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Rayon Sports, lakini mipango hiyo imefutwa rasmi. Uongozi wa klabu umethibitisha kuwa maboresho makubwa yaliyofanyika Avic Town yameondoa haja ya kusaka kambi nje ya mipaka ya Tanzania.
“Tumefuta hiyo safari. Kwenye kambi yetu kulikuwa na ukarabati mkubwa umefanyika. Hata kama tungetoka nje ya nchi, tungeishia kurudi pale. Kwa mabadiliko yaliyofanyika, tumekubaliana tutamalizia maandalizi yetu hapo, na uzuri kocha ameridhia,” alisema mmoja wa mabosi wa juu wa Yanga.
Kihistoria, kila msimu ambao Yanga imeweka kambi Avic Town umekuwa wa mafanikio. Wananchi wamefanikiwa kutwaa makombe yote ya ndani kila walipoweka kambi hapo, isipokuwa mara moja tu ambapo hawakunyakua Ngao ya Jamii.
Hali hii imeendelea kuipa uhalali Avic Town kama kituo chenye bahati na hamasa kubwa kwa mabingwa hao wa Tanzania Bara, jambo ambalo pia limechangia uongozi kutokuwa na shauku ya kutafuta maandalizi nje ya nchi.