Kocha Romain Folz ametimiza mwezi mmoja tangu alipoanza kukinoa kikosi cha Yanga akichukua nafasi iliyoachwa na Miloud Hamdi aliyetimkia klabu ya Ismailia ya Misri
Folz alianza rasmi majukumu ya kuinoa Yanga August 01 ambapo mabingwa hao wa Tanzania Bara walianza maandalizi ya msimu mpya 'pre-season'
Wiki mbili za kwanza kikosi chake kilijifua dimba la KMC Complex kabla ya kuhamia Avic Town ambapo kwa misimu minne sasa Yanga imeweka makazi hapo
Chini ya Folz, Yanga imecheza mechi kadhaa za kirafiki ikifanikiwa kupata ushindi katika mechi hizo. Yanga ilibeba taji la Rayon Sports Day baada ya kuichapa Rayon Sport mabao 3-1 nchini Rwanda.
Waliporejea nchini, Wananchi pia wakacheza mechi nyingine za kirafiki dhidi ya Fountain Gate ambapo waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kisha kuichapa Tabora United mabao 4-0
Folz amewahakikishia mashabiki wa Yanga kuwa kikosi chake kitakuwa tayari baada ya pre-season na watakwenda kupambania ushindi katika kila mashindano watakayoshiriki msimu ujao
Yanga inatarajiwa kucheza mechi kadhaa za kirafiki kabla ya kilele cha Wiki ya Mwananchi Septemba 12 ambapo watacheza dhidi ya Bandari Fc ya Kenya
Mchezo wa kwanza wa kimashindano kwa Folz ni dhidi ya Simba, Septemba 16 ukiwa ni mchezo wa Ngao ya Jamii ambapo baada ya mchezo huo Yanga itasafiri hadi Angola kuifuata Wiliete Banguela katika mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa Septemba 21 na kurudiana jijini Dar Septemba 28.