Klabu ya Yanga imesema haifanyi utani kuelekea mchezo wa Ngao ya Jamii, hivyo Kocha Mkuu, Romain Folz, amekuwa na 'programu' nne tofauti za maandalizi kuelekea mechi hiyo inayotarajiwa kupigwa, Septemba 16, mwaka huu, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema kocha wa timu hiyo amekuwa na mazoezi ya gym, ufukweni, uwanjani na darasani kwa ajili ya mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba ambao utakuwa unaashiria kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu mpya, Septemba 17, mwaka huu.
Kamwe amesema kocha Romain anataka kuendeleza rekodi za makocha wenzake, Miguel Gamondi na Miloud Hamdi, ambao walikuwa wakiisulubu Simba kila wanapokutana.
Alisema anataka kuendeleza rekodi ya Yanga kuifunga Simba, ambapo kama atafanikiwa itakuwa ni mara ya sita mfululizo kwa timu yao kuwafunga watani wao wa jadi.
"Timu inaendelea vizuri kumekuwa na programu tofauti tofauti za uwanjani, gym, ufukweni na darasani, huu ni mwendelezo wa maandalizi hasa kuelekea kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, ingawa tuna mchezo dhidi ya Bandari ya Kenya kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi"
"Mwalimu ni mpya na wasaidizi wake ni wapya, hilo linakupa picha kwamba wanataka kufanya vizuri. Mwalimu nimemwangalia ana vitu vingi, ana mbinu nyingi sana ambazo zitaanza kuonekana Wiki ya Mwananchi, Ngao ya Jamii na hata kwenye michezo ya kimataifa," alisema Kamwe.
Katika mchezo wa Septemba 16, Yanga inajivunia rekodi yake bora dhidi ya watani zao wa jadi. Imefanya hivyo mara tano kwenye makombe tofauti.
Mara ya mwisho iliifunga Simba mabao 2-0, katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, uliochezwa Juni 25, mwaka huu, Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kabla ya hapo, ilishinda mabao 5-1, mechi ya mzunguko wa kwanza Ligi Kuu msimu wa 2023/24, Novemba 5, 2023, ikishinda tena 2-1, mechi ya mzunguko wa pili msimu huo, Aprili 20, 2024.
Yanga iliidungua tena Simba, bao 1-0, Agosti 8, mwaka jana, katika mchezo wa Ngao ya Jamii, kabla ya kupata ushindi wa 1-0 kwa mara nyingine, Oktoba 19, mwaka jana, katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu.
Kamwe pia amesema kikosi hicho pia kinaendelea na maandalizi ya mchezo wa awali, Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete FC ya Angola, utakaopigwa jijini Luanda, Septemba 21, mwaka huu.
Alisema lengo ni lile lile kuhakikisha inatimiza lengo namba moja la klabu hiyo ambalo ni kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo ya kimataifa. Ikumbukwe kuwa msimu uliopita, Yanga iliishia hatua ya makundi, iliposhika nafasi ya tatu kwenye Kundi A, ikiishia na ponti nane, na kuziacha timu za Al Hilal ya Sudan na MC Alger ya Algeria, zikisonga mbele.