Klabu ya Yanga SC imekamilisha taratibu za kiserikali na kupatiwa umiliki wa eneo la ujenzi wa uwanja wake mpya utakaokuwa Jangwani, Dar es Salaam, eneo lenye takribani mita za mraba 37,500.
Taarifa zinaeleza kuwa hatua za awali za mchakato wa ujenzi zimeanza, ikiwemo maandalizi ya kutangaza tenda kwa ajili ya kumpata mkandarasi atakayejenga uwanja huo. Uwanja huo unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki wapatao 30,000.
Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, hivi karibuni alifanya ziara nchini Brazil ambapo pamoja na mambo mengine, aliitumia ziara hiyo kujifunza uzoefu na taratibu za ujenzi wa viwanja vya kisasa, ikiwa ni maandalizi ya kuhakikisha ujenzi wa uwanja wa Jangwani unakidhi viwango vya kimataifa.
Uwanja huo utajengwa katika eneo ambalo awali ulikuwapo Uwanja wa Kaunda, huku Serikali ikiongeza eneo zaidi kufuatia kuridhia kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan.
Kupatikana kwa uwanja huo kunatarajiwa kuongeza hadhi ya Yanga na kutoa fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na ajira na shughuli za kibiashara zitakazohusiana na uwanja huo.