Rais wa Yanga Injinia Hersi Said amesema Yanga ndio klabu yenye thamani kubwa zaidi nchini kwa kuzingatia mali ambazo klabu hiyo inamiliki. Hersi alitoa kauli hiyo jana wakati akizindua tawi la NSSf Yanga Family jijini Dar es salaam
Siku chache zilizopita katika Mkutano Mkuu wa Wanachama wa Yanga, Kamati maalum chini ya Alex Mgongolwa iliyopewa jukumu la kuipa thamani klabu ya Yanga, ilitangaza thamani ya klabu ni Tsh Bilioni 100
Mijadala mingi imeibuka ambapo wapo waliohoji usahihi wa thamani hiyo wakifananisha na klabu nyingine kubwa barani Afrika kama Al Ahly na Mamelodi Sundowns
"Hakuna klabu tajiri kama Yanga hapa Tanzania. Yanga ndio klabu yenye mikataba mikubwa kuliko zote, maana yake thamani ya kibiashara sisi ni namba moja"
"Sisi tuna mali zisizohamishika, tuna jengo pale Jangwani lakini pia sisi tuna jengo jingine liko mtaa wa Mafia, Kariakoo hapa Dar es salaam"
"Nitafutieni klabu nyingine yenye majengo mawili Kariakoo, Hakuna. Sisi tuna ardhi hapa Jangwani, ardhi hii ina sqm 37,500 ambayo kwa thamani yake ya sasa inafikia Bilioni 56"
"Pia tuna eneo liko Kigamboni ambalo tunaweza kulitumia kujenga viwanja vya mazoezi, kama tukiendeleza eneo hili pengine tunaweza kutumia Bilioni 3. Tukitoa thamani hiyo katika eneo letu la Jangwani tunaweza kubaki na Tsh Bilioni 53"
"Tunaposema hii ni klabu namba moja kwenye utajiri tunamaanisha ni pamoja na mali zote tunazomiliki," alisema Hersi