Wakati Yanga ilipoweka hadharani kikosi cha kuikabili Simba katika mchezo wa Ngao ya Jamii jana, jina la kiungo Aziz Andabwile lilipenya katika orodha ya wanaume 11 ambao kocha Romain Folz aliwapa jukumu la kuwakilisha Wananchi katika mchezo huo
Andabwile alikabidhiwa mikoba iliyoachwa na Khalid Aucho, Folz akianza na kikosi kilekile kilichoichapa Simba mabao 2-0 katika mechi ya kuhitimisha msimu uliopita na kuihakiikishia Yanga ubingwa wa ligi kuu ya NBC
Wapo mashabiki 'walimaliza maneno' kwa kuliona jina la Andabwile katika orodha ya nyota wanaoanza lakini baada ya dakika 90 za mchezo huo ambao Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 habari imebadilika
Andabwile amewashangaza wengi kwa kiwango alichoonyesha katika mchezo huo, pengine rasmi baada ya dakika 90 za mchezo wa jana, wale waliokuwa wanatamani kumuona Khalid Aucho akirejeshwa tena Jangwani, watafuta mawazo hayo
Andabwile amelitendea haki eneo la kiungo mkabaji, hapa kongole kwa uongozi wa Yanga chini ya Rais Injini Hersi Said ambaye katika dirisha hili alimuongezea Andabwile mkataba wa miaka miwili kinyume na matarajio ya wengi ambao waliamini angekuwa miongoni mwa wachezaji ambao wangepewa Thank You
Lakini pia ujasiri alioonyesha Folz kwa kumtumia Andabwile katika mchezo huo umemlipa kwani kama mambo yangekwenda tofauti Folz angebeba mzigo wa lawama
Andabwile amekuwa na nyakati bora kwenye kikosi cha Yanga tangu ujio wa Folz, ametumika katika mechi zote za kirafiki ambazo Yanga ilicheza wakati wa pre-season
Anaonekana kuelewa mfumo wa uchezaji wa Folz kwa haraka kwani hata katika mchezo dhidi ya Simba jana, mara kadhaa alionekana akiwaelekeza wenzake pale nyuma jinsi ya kujipanga timu inapokuwa na mpira au bila ya mpira
Bila shaka Moussa Balla Conte aliyetarajiwa kuwa chaguo la kwanza katika safu ya kiungo mkabaji, ana kazi ya kufanya mbele ya Andabwile ambaye ni kama ameibuka kutoka kusikojulikana...!