Klabu ya Simba SC imethibitisha kuachana na aliyekuwa kocha wao mkuu, Fadlu Davids, aliyejiunga na timu hiyo tangu msimu uliopita. Uamuzi huu unakuja baada ya matokeo mabaya mfululizo, hususan dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga SC.
Kwa mujibu wa taarifa, Fadlu alifikia hatua ya kuondoka mara baada ya kupoteza mchezo wa Ngao ya Jamii kwa bao 1-0 dhidi ya Yanga wiki iliyopita.
Huo ulikuwa mchezo wa nne mfululizo ambao Fadlu amepoteza mbele ya Yanga, na kwa Simba, kilikuwa kipigo cha sita mfululizo dhidi ya watani wao hao wa jadi, rekodi ambayo imekuwa ikiumiza mashabiki wa Msimbazi kwa kiwango kikubwa.
Mzozo ulianza kuzidi moto baada ya Ngao ya Jamii, huku presha kutoka kwa mashabiki na wadau ikionekana kuongezeka. Kwa wengi, unaweza kusema kocha wa Yanga, Romain Folz, ndiye chanzo cha maumivu Msimbazi. Kila mara Yanga inapoibuka na ushindi, inakuwa balaa upande wa pili wa mto Msimbazi.
Kauli ya mashabiki wa Yanga kwamba 'msimu huu wanapiga utosini' sasa inaonekana kuchukua sura ya kweli. Kila ushindi wao dhidi ya Simba umekuwa na athari kubwa, si tu kwa wachezaji bali hata kwa benchi la ufundi na utulivu wa klabu yao.
Kwa sasa, Fadlu Davids anatajwa kujiunga na Raja Casablanca ya Morocco akiiacha Simba ikihaha kusaka kocha mpya