Klabu ya Yanga SC imeendelea kuthibitisha ubora wake kwenye Ligi Kuu ya NBC na mashindano mengine baada ya kufikisha mechi 33 mfululizo bila kupoteza.
Juzi, Yanga ililazimishwa suluhu ya bila kufungana dhidi ya Mbeya City kwenye mchezo wa ligi kuu uliopigwa Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.
Ingawa matokeo hayo hayakuwafurahisha mashabiki wa Wananchi ambao wanahisi kikosi hakijafika katika ubora wa msimu uliopita, takwimu zinaonyesha kuwa Yanga imekuwa timu ngumu kufungika.
Kwa mujibu wa rekodi, mara ya mwisho Yanga kupoteza mchezo ilikuwa Desemba 07, 2024, katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ilipofungwa mabao 2-0 na MC Alger huko Algeria.
Upande wa Ligi Kuu, Yanga mara ya mwisho kuonja machungu ya kipigo ilikuwa Novemba 07, 2024, ilipofungwa mabao 3-1 na Tabora United kwenye dimba la Azam Complex.
Baada ya kipigo hicho, Wananchi walihamia kutumia Uwanja wa KMC Complex na tangu hapo hawajapoteza mchezo wowote wa ligi, wakiwa na takribani mechi 22 mfululizo bila kupoteza.
Hii si mara ya kwanza Yanga kuweka rekodi za kipekee. Misimu miwili iliyopita, klabu hiyo iliweka historia ya kucheza mechi 49 bila kupoteza katika mashindano yote, rekodi ambayo bado ni kumbukumbu ya fahari katika soka la Tanzania.
Licha ya mashabiki kutoridhishwa na mwanzo wa msimu huu, Yanga ipo kwenye nafasi nzuri ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo itakabiliana na Silver Strikers ya Malawi katika mechi mbili (nyumbani na ugenini) kuwania tiketi hiyo.
Aidha, baada ya michezo miwili ya Ligi Kuu, Wananchi wanashikilia nafasi ya nne kwenye msimamo wakiwa na alama nne alama mbili nyuma ya watani zao Simba wanaoongoza ligi na alama sita. Bado ni mapema sana kwani ndio kwanza ni mechi mbili tu zilizochezwa